Advertisements

Tuesday, November 18, 2014

Maswali Kumi kwa Mbunge wangu:Makongoro Mahanga

Makongoro Mahanga
1. Shomari Kitogo, mkazi wa Segerea
Barabara hasa kutoka Segerea Mwisho hadi Makaburini ambako ni nyumbani kwako ni mbovu, nataka unipe maelezo ya kina na yenye matumaini ya utekelezaji ili unishawishi kukupa kura yangu katika uchaguzi ujao.
Jibu: Kuna miradi mingi ya barabara na madaraja iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) katika Kata ya Kinyerezi, barabara ya kutoka Segerea-Kinyerezi hadi Majumba Sita imekamilika kuboreshwa kwa lami na wakala huyo katika kipindi hiki.
Pia, Tanroads imekamilisha daraja kubwa la Segerea/Kinyerezi na imeanza ujenzi wa daraja jingine kubwa la Kinyerezi/Sitakishari. Tanroads pia imekuwa ikikarabati Barabara ya Kinyerezi-Kifuru-Malambamawili kwa changarawe huku mipango ya kuanza kujenga barabara hiyo kwa lami ikiwa imekamilika na ujenzi utaanza wakati wowote kwa kipande cha Kinyerezi hadi Kifuru. Barabara nyingine inayosimamiwa na wakala ni ya Kimara - Bonyokwa hadi Kinyerezi Shule. Nimeshaiagiza Tanroads ikarabati barabara hiyo kwani iko katika hali mbaya.
2. Stella David, mkazi wa Tabata
Sijawahi kukuona hata siku moja. Ningekuwa nimekuona ningetaka unieleweshe sababu za kutokuwa na maji kwa miaka yote hii. Sidhani kama mimi nitakuwa mpigakura wako labda nitakapopata jibu la uhakika ni lini tutapata maji?
Jibu: Natembelea jimboni mara kwa mara na kipindi hiki kuanzia Julai 5 hadi 26, nilitembelea Kata zote nane za jimbo langu na kufanya mikutano ya hadhara. Ninachoweza kusema ni kwamba wapigakura wangu wasidhaharau matangazo wanaposikia wajongee na waniulize maswali nitawajibu na yakibaki nitapanga siku ya kukutana nao na kuwaelewesha.
3. Salmini Myemba, makazi Kinyerezi
Kuna baadhi ya maeneo yamejengwa kiholela, hakuna kinachofanyika kuhakikisha kunakuwa na mitaa inayopitika, nahitaji ufafanuzi suala hilo utalifanyia kazi lini na mchakato wake ukoje? Vilevile, suala la michango shuleni limekuwa tatizo nataka anipe ufafanuzi litakwisha lini kwa sababu Serikali imetangaza kuwa elimu ni bure.
Jibu: Mitaa mingi imejengwa siku nyingi, ninachoweza kusema watu wa Mipango Miji hawakuliona hilo tangu awali. Mimi kama Mbunge inakuwa ngumu kutatua kero hiyo kwa kuwa sina fedha za kuwalipa ili nipitishe bomoabomoa kunyoosha mitaa.
Kwa hiyo ninachofanya sasa ni kuhakikisha wanaojenga kipindi hiki wanafuata utaratibu katika ujenzi wakizingatia barabara na kutojenga kwenye mkondo wa maji kwani mara nyingi ujenzi huo ndiyo unaosababisha mafuriko na wapo watu wameshapewa onyo mara kadhaa licha ya kuwa viwanja ni vyao.
4. Asha Said, mkazi wa Tabata Bima
Katika jimbo letu vikoba ni mtihani, hakuna juhudi unazofanya ukishirikiana na watendaji wako kuhakikisha tunapata mikopo ya kujikomboa. Kama unataka kura yangu, nipe maelezo ya kina na nikuelewe.
Jibu: Miongoni mwa mambo niliyowahi kuyatolea ufafanuzi mara nyingi tena katika mikutano ya hadhara ni kuwataka kina mama kuungana katika vikundi na kuwasilisha maombi yao.
Nitakuwa na nafasi nzuri ya kuwasaidia wakiwa wameungana na ninakuruhusu uzunguke kwa kina mama walioungana na kuhitaji mikopo ukimpata aliyenyimwa, njoo uniulize tena, kwani nina uhakika hakuna na ninaweza kusem jimbo langu linaongoza kwa kina mama kujishughulisha katika vikundi na kupatiwa mikopo.
5. Janeth Msami - Mkazi wa Gongolamboto
Kero ya michango shuleni, mtoto anasoma nusu mwezi kila siku anarudishwa kibaya zaidi kila mwaka tunachangia madawati lakini bado kuna watoto wanakaa chini. Mbunge ni kwa jinsi gani unalifanyia kazi tatizo hili?
Jibu: Michango shuleni siyo ya ada ni ile ambayo wanakubaliana kati ya wazazi na kamati za shule, hivyo lipo chini ya makubaliano hayo. Hapa labda nitoe angalizo tu kuwa wazazi wanatakiwa kuhudhuria mikutano ya shuleni ili vitu muhimu kuhusu elimu ya watoto wao vinapojadiliwa wawepo. Hili limekuwa linaleta manung’uniko mengi kwa wazazi kutokana na kuambiwa elimu ni bure na wanasahau kuwa kuna masuala ambayo wazazi wanatakiwa kuchangia ikiwamo masomo ya ziada.
6. Maze Moshi, mkazi wa Tabata Kimanga
Utendaji wako wa kazi hauridhishi. Jipange kulitembelea jimbo lako kama vipi uache kimoja kama unataka kuwa mbunge uwe mbunge, ukitaka kuwa waziri uwe waziri kwa sababu huonekani jimboni.
Jibu: Kuwa waziri na mbunge hakunizuii kufanya mambo yangu, ingawa kuna wakati nakiri ninakuwa na kazi nyingi kiasi kwamba nalazimika kuacha majukumu kwa watendaji wengine.
Kutekeleza majukumu ni wajibu wangu bila kujali nipo wapi, lakini kuhusu kufika jimboni kama nilivyokwishasema hapo awali, siyo kweli kwamba sifiki, ninajitahidi kuzunguka katika kata zote nane na kukutana na wananchi, kama ambavyo nimefanya mapema mwaka huu na huo ni utaratibu wangu wa miaka yote.
7. Gidion Lameck, mkazi wa Tabata Shule
Uliahidi kuboresha ajira kwa vijana. Nataka kufahamu hali hii hadi lini?
Jibu: Tatizo la ajira ni kubwa na siyo Tanzania pekee, bali duniani kote. Ndiyo maana tunajitahidi kuhakikisha vijana wanapokuwa shuleni wanajifunza kujiajiri badala ya kuwekeza akili katika kuajiriwa. Lakini ukija ofisini kwangu utakuta ushahidi wa mafaili ya vijana wanaoomba niwasaidie kuwaunganisha katika kazi mbalimbali na mara mojamoja ninapopata nafasi za kuwaweka ninafanya hivyo.
Ushauri wa bure, waungane katika vikundi ili niangalie ni namna gani ninaweza kuwasaidia na wao wakajisaidia kwa kuwapa semina na mitaji kwa wanatakaokuwa na nia ya kufanya biashara, lakini kuwapa ajira mmojammoja ni ngumu kwani vijana wapo wengi na ofisi zenye kazi au kampuni zenye nafasi zipo chache.
8. Emmanuel Sanga, mkazi wa Vingunguti
Umewasahau wapigakura wako, ukija huku unakutana na wanaCCM wenzako unaondoka. Kwa nini tangu tumekuchagua huji kusikiliza malalamiko yetu hadi waandishi wakuulizie?
Jibu: Siyo kweli kwamba nakutana na wanaCCM, kinachotokea kama wanachama, mbunge wao anapokuwa kwenye mkutano na wananchi lazima watafika kwa wingi wakiwa wamevaa sare, hivyo kuonekana kama nimekwenda kuzungumza na wao.
Namshauri mwananchi wangu mpigakura wangu, afike katika mikutano yangu bila kujali wamejaa watu wa aina gani na kama ana swali lolote aniulize, nitampa majibu palepale.
9. Jonas Mahimbo, mkazi wa Vingunguti
Huku maeneo ya Vingunguti miundombinu ni mibovu. Barabara nyingi zipo katika hali mbaya. Je, una sifa ya kuendelea kuwa mbunge?
Jibu: Sifa ninayo kutokana na juhudi ninazofanya kutatua tatizo hilo ikiwamo miradi ya miundombinu iliyotekelezwa katika Kata ya Vingunguti. Ujenzi wa daraja kubwa la Vingunguti/Segerea limekamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh2 bilioni. Miradi ya miundombinu chini ya mradi wa CIUP ikiwamo ujenzi wa barabara ya lami kutoka Barabara Kuu ya Nyerere hadi Vingunguti Darajani na ile ya Mtaa wa Miembeni ilikamilika pia katika kipindi hiki. Barabara nyingine za changarawe katika Kata ya Vingunguti chini ya mradi huu pia zilikamilika ikiwamo ya kuelekea Majengo na Mji Mpya. Tumemteua I.K. Andersen Contractors kukarabati barabara ya Vingunguti Relini – Karakata (Ng’ombe Road) kwa gharama ya Sh43,108,590 na kazi hiyo itaanza hivi karibuni.
10. Mage Sheki, mkazi wa Ukonga
Maji ni tatizo sugu katika jimbo hili hakuna mkazi asiyelalamikia maji. Je, ni lini tutapata maji kama wenzetu wa majimbo mengine?
Jibu: Tatizo la maji bado ni kubwa Kata ya Kinyerezi. Hata hivyo, kuna miradi inayoendelea ya kuchimba visima, ukiwamo mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji na Umoja wa Ulaya (EU/BTC) katika eneo la Kanga. Mradi huu umekamilika isipokuwa tatizo ni umeme mdogo. Tayari Tanesco wameombwa kurekebisha hali hiyo. Pia katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wa miradi ya visima katika vijiji 10 kila wilaya, Kata ya Kinyerezi itachimbiwa visima viwili maeneo ya Bonyokwa na Kifuru. Pia kuna Sh30 milioni ambazo zitatumika kutafutia chanzo kingine cha maji mazuri. Tatizo la Kata ya Kinyerezi ni kukosekana kwa maeneo mengi yenye maji mazuri na ya kutosha. Mbali na mradi mkubwa wa maji wa Dawasa kutoka Ruvu Juu kukamilika Septemba, 2015 tatizo la maji katika Jimbo la Segerea ikiwamo Kata ya Kinyerezi litakwisha.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

mbona unaongelea kinyerezi na kifuru tu?tabata na segerea hatui maji ya bomba tangu mchina atuunganishie mabomba tu hakuna maji.ila chakushangaza siku kuna mkutano wa ccm ndio tunafunguliwa maji kutwa nzima.je kwa nini maji yasifunguliwe angalau mara tatu kwa wiki ni mpaka mkutano ufanyike ndio tupewe maji?

Anonymous said...

Mheshimiwa Mbunge, unapendeza sana na shati la pink. Vipi kuna wabunge wenzako wanaopenda pink?