Advertisements

Wednesday, September 28, 2016

22 WATIWA MBARONI KWA TUHUMA ZA KUTAKA KUCHOMA MOTO OFISI ZA CUF DAR ES SALAAM

Ikiwa zimepita siku kadhaa tangu Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutuhumu baadhi ya viongozi wake waliosimamishwa uanachama kupanga njama za utekaji viongozi wa chama hicho, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikiliwa wanachama wa CUF 22 kwa tuhuma za kupanga njama za kufanya fujo na kuchoma mali za ofisi za chama hicho.

Ikumbukwe kuwa, Septemba 16,2016 CUF kupitia Kurugenzi yake ya Habari na Uenezi ilitoa taarifa ya jaribio la utekaji wa Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha CUF, Joran Bashange ambapo chama hicho kiliwatuhumu Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya na Profesa Ibrahim Lipumba kuwa walinzi wao walijaribu kufanya tukio hilo.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro jana alisema wanachama hao walikamatwa na zana za kufanyia uhalifu yakiwemo mapanga, Jambia, visu na chupa za kupulizia 10 zikiwa kwenye boksi lenye maandishi ya lugha ya kichina.

Watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 25,2016 maeneo ya Mwananyamala katika gari ya abiria ambayo ruti yake inapitia njia ya Buguruni-Mwananyamala.

Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya askari kupata taarifa kwamba wamekuja Dar es Salaam wakitokea visiwani Unguja kutoka katika matawi mbalimbali ya chama hicho kwa lengo la kufanya fujo.

Aidha, Sirro alisema baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa, walieleza kuwa wamekuja kutokana na maelekezo ya kiongozi wa CUF Nassoro Ahmad Mazrui ambaye ni Naibu Katibu mkuu wa chama hicho aliyewataka kuungana na walinzi wenzao waliopo katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni.

Hata hivyo, baada ya taarifa za watuhumiwa hao kukamatwa kuenea katika mitandao ya kijamii, baadhi ya watu walimhusisha aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa CUF kwa muda Julias Mtatiro kuhusika katika mipango ya njama hizo.

Lakini Kamanda Sirro alieleza kuwa hadi sasa hajapokea taarifa hiyo ya kuhusika kwa Mtatiro na kwamba taarifa hizo si za kweli.

No comments: