Advertisements

Tuesday, December 6, 2016

SERIKALI YATAKIWA KUBAINISHA STENDI ZA DALADALA JIJINI MWANZA

 Mwenyekiti wa Madereva Kanda ya ziwa Hassan Dede akihojiwa na waandishi wa habari
Askari wa kikosi cha usalama barabarani wakiwa wamezisimamisha Daladala kwa kosa la kupakia abira eneo ambalo sio rasmi

 Jinsi magari yanavyogeuza katika eneo la Buhongwa
 Eneo la stendi isiyokuwa rasmi ya Buhongwa ilivyo katika kadhia ya ubovu
 Mwenyekiti wa Madereva Kanda ya ziwa Hassan Dede akikagua eneo la barabara ya Buhongwa ambayo inatumiwa na madereva Daladala kama stendi
 Gari likigeuza katikati ya barabara kutokana na kukosekana kwa eneo maalumu la stendi


 Wajasiriamali wakiwa katika eneo la biashara huku Daladala zikitumia eneo hilo pia kupakia na kushusha abiria
 Gari inageuza kituoni ambapo ni barabarani huku watu wakiendelea kuvuka barabara
 Dede akikagua barabara iliyoharibika
 Gari ikiwa imepaki katika eneo bovu la barabara ya Buhongwa



 Mwandishi wa habari wa www.wazo-huru.blogspot.com Mathias Canal akimhoji moja ya madereva katika eneo la Buhongwa

 Mwenyekiti wa madereva Kanda ya ziwa Bw Hassan Dede akisalimia na wakazi wa eneo la Nyashishi mara baada ya kuzuru katika eneo hilo ambalo ndilo amependekeza kuwa stendi ya daladala, kushoto kwake ni Mwandishi wa habari wa www.blogspot.com Ndg Mathias Canal

Na Mathias Canal, Mwanza

Uongozi wa Mkoa wa Mwanza umetakiwa kubainisha stendi za Daladala, maeneo maalumu kwa ajili ya kufanyia biashara za mbogamboga na matunda kwa kina mama sambamba na kubainisha maeneo maalumu ambayo daladala haziruhusiwi kusimama kwani kufanya hivyo kutaondoa urasimu uliopo baina ya madereva wa Daladala na askari wa usalama barabarani.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa madereva Kanda ya ziwa Bw Hassan Dede wakati alipozuru kujionea kadhia wanazokumbana nazo madereva wawapo barabarani sambamba na kujionea kandia wanayoipata kutokana na ubovu wa barabara na kutokuwa na stendi ya Daladala katika Mtaa wa Buhongwa nje kidogo ya Halmashauri ya Manispaa ya Nyamagana.

Dede alisema kuwa ni ajabu kwa nchi yetu kuwa na kituo cha daladala chenye mwanzo lakini hakina mwisho hivyo kuwafanya madereva kugeuza mahala pasipokuwa rasmi ambapo ni hatari kwa uhai na magari na madereva hao.

Katika eneo la Buhongwa zinapogeuzia daladala kama kituo, barabara yake ni mbovu huku pembeni kukiwa na machinga sambamba na wajasiriamali wanaouza mbogamboga na matunda jambo ambalo linaweza kusababisha hatari kwa wafanyabiashara hao endapo kama gari litaharibika kutokana na hitilafu ya breki.

Hata hivyo alisema kuwa kumekuwa na wimbi la ukamataji na kutozwa faini na askari wa usalama barabarani kwa madereva hao kutokana na kuegesha magari katika eneo la barabara kwa ajili ya kupakia abiria jambo ambalo ni kinyume na utaratibu kwani hakuna kituo katika eneo hilo pamoja na madereva hao kulipia ushuru kila siku.

Dede alisema kuwa katika njia itokayo Kishiri, Airport, Ilemela na Kisesa kuelekea Buhongwa kuna jumla ya Daladala 1900 ambayo kwa siku moja kila gari inalipia ushuru wa shilingi 1000 ambapo kwa gari zote 1900 kwa siku serikali inakusanya kodi ya jumla ya shilingi 1,900,000/=.

Katika kipindi cha mwezi mmoja serikali inakusanya jumla ya shilingi 57,000,000/= huku ikiwa inakusanya jumla ya shilingi 693,500,000 kwa mwaka.

Dede amehoji fedha zote hizo serikali inafanyia nini kama imeshindwa kukarabati barabara itokayo Mwanza Mjini kuelekea Airport sambamba na kukarabati na kubainisha eneo maalumu la stedi kwa ajili ya Daladala.

Sambamba na hayo pia Dede amependekeza serikali kuhamisha kituo cha daladala kisichokuwa rasmi cha Buhongwa kuhamia katika eneo la Nyashishi lililopo mwanzoni mwa Wilaya ya Misungwi kwani kupitia kuwepo kwa eneo hilo daladala zote zitafanikiwa kuingia katika stendi hiyo na serikali itakusanya mapato mengi kwani itakuwa rahisi kuwabana madereva wote.

Katika Barabara itokayo Makao makuu ya Mkoa wa Mwanza (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa) kuelekea eneo hilo la Buhongwa kuna vituo rasmi visivyopungua sita huku vituo visivyo rasmi vipo zaidi ya 15 hivyo ni vyema uongozi wa Mkoa wa Mwanza kupitia ofisi ya usalama barabarani kusimamia jambo hilo na kuweka alama mahususi zitakazobainisha vituo hivyo.

MWISHO

No comments: