Advertisements

Saturday, March 25, 2017

MAKAMANDA WA POLISI KUPANGA MIKAKATI YA KUPAMBANA NA UHALIFU DODOMA.

Msemaji wa Jeshi la Polisi,  Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Advera Bulimba 

Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Maofisa wakuu wa Polisi  wanatarajia kukutana mkoani Dodoma kuanzia jumatatu tarehe 27 mpaka  tarehe 29 mwezi wa tatu mwaka huu, katika kikao kazi cha siku tatu kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu hapa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, Msemaji wa Jeshi la Polisi,  Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Advera Bulimba alisema kikao hicho kitawakutanisha maofisa wakuu wa makao makuu ya Polisi, makamanda wa Polisi wa mikoa na Makamanda wa vikosi vya bara na Zanzibar ili kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utendaji katika kipindi cha mwaka uliopita na kuweka mikakati mipya ya kupambana na uhalifu kwa mwaka 2017.
Aidha, Bulimba alisema mbali na utaratibu wa mawasiliano ya kila siku katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Jeshi la Polisi pia lina utaratibu wa kukutana kila mwaka kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu wa kukabiliana na wahalifu kwa lengo la kuhakikisha kuwa usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika hapa nchini.
“Katika kikao hicho Inspekta Jenerali wa Polisi IGP Ernest Mangu atatoa maelekezo ya kiutendaji ambayo lengo lake ni kuhakikisha kuwa kila ofisa,  mkaguzi na askari anawajibika kwa nafasi yake katika kuhakikisha uhalifu unapungua hapa nchini” Alisema Bulimba.
Bulimba alisema kikao kazi hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ambapo kauli mbiu katika kikao hicho ni “Zingatia maadili tunapopambana na uhalifu ili kuimarisha usalama kwa maendeleo ya Taifa”.

No comments: