Advertisements

Sunday, August 20, 2017

Katibu Soko la Sido ashikiliwa kwa uchochezi

Mfanyabiashara wa Soko la Sido mjini Mbeya akilalamikia kitendo cha Serikali kuwazuia kujenga vibanda vya kudumu ndani ya soko hilo lililoteketea kwa moto.Picha na Godfrey Kahango 

Wakati hali ya amani na utulivu ikiwa imerejea katikati ya Jiji la Mbeya baada ya kutokea vurugu juzi mchana, jeshi la polisi limesema linawashikilia watu 18 akiwamo Katibu wa Wafanyabiashara wa Soko la Sido, Alanus Ngogo kwa tuhuma za kuchochea vurugu hizo.
Juzi mchana, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na upupu kuwatawanya wanafabiashara wa soko hilo waliokuwa wamegoma kutekeleza agizo la Serikali la kuwataka kutoendelea na ujenzi wa vibanda vya kudumu ndani ya soko hilo ambalo liliteketea kwa moto na kuunguza mali zote usiku wa kuamkia Agosti 15 mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga aliliambia gazeti hili jana kwamba baada ya kutokea kwa vurugu kuna watu waliokuwa katika soko hilo la Sido waliingia na kufunga barabara kuu ya Tanzania-Zambia kwa mawe na magogo huku wakipiga mawe magari yaliyokuwa yakipita.
“Katika tukio la juzi tuliwakata watu 18 hawa kosa lao ni kuingia barabarani na kuanza kupanga mawe na magogo na kuzuia magari yasipite barabara kuu ya Tanzania-Zambia kuanzia Kabwe hadi Mafiati.
“Lakini yule katibu wa soko (Alanus Ngogo) yeye anatuhumiwa kwa kosa la uchochezi kwani juzi ile mimi nilipopanda jukwaani na kuwataka watu wote waende nyumbani kwao kwa usalama wao yeye alichukua kipaza sauti na kuanza kuwahamasisha watu wasiondoke eneo lile akitamka ‘tutakesha hapa hapa’ na maneno mengine ya kukashifu,” alisema Kamanda Mpinga.
Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na baada ya kumalizika kwa mahojiano watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zao.
Kuhusu hali ya usalama, Kamanda Mpinga alisema ulinzi katika jiji hilo umeimarishwa na polisi wapo doria muda wote na watu waliamka alfajiri kuendelea na shughuli zao maeneo mengi hususan Soweto, Kabwe, Manjelwa hadi Mafiati ambako juzi biashara zilifungwa kutokana na usalama kuwa mdogo.
Hata hivyo, Serikali ya Mkoa wa Mbeya kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ilisisitiza kusimamia msimamo wake wa kutowaruhusu wafanyabiashara hao kuendelea na ujenzi wa vibanda vyao tofauti na ombi lao kutaka kuruhusiwa.
Ntinika aliwataka wafanyabiashara hao kuwa na hali ya utulivu na uvumilivu kwa kusubiri siku tano zilizotengwa na Serikali ili kupisha kamati maalumu iliyoundwa kufanya tathmini ya hasara iliyojitokeza kutokana na janga hilo pamoja na kuchunguza kiini cha moto huo.

Chanzo: Mwananchi

No comments: