Advertisements

Saturday, October 21, 2017

MAHAFALI YA KWANZA YA KIDATO CHA NNE KWA WAATHIRIKA WA NDOA NA MIMBA ZA UTOTONI SHULE YA AGAPE KNOWLEDGE OPEN SCHOOL YAFANA


Ijumaa Oktoba 20,2017 kumefanyika Mahafali ya Kwanza ya Kidato cha nne shule ya Sekondari “Agape Knowledge Open School” ambapo jumla ya watoto yatima na waathirika wa ndoa na mimba za utotoni 29 wanahitimu masomo yao kupitia mfumo wa elimu usio rasmi mwaka huu. 

Mahafali hayo yamefanyika katika shule hiyo iliyopo katika mtaa wa Busambilo kata ya Chibe manispaa ya Shinyanga na mgeni alikuwa Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Shinyanga,James Malima kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack. 
Awali akizungumza wakati wa mahafali hayo,Mkuu wa shule hiyo ,Adili Haruni Nyaluke alisema wanafunzi hao walianza masomo yao mwaka 2014 wakiwa 54 wote wasichana na wanaohitimu ni 29. 
Naye Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP),linalomiliki shule hiyo,John Myola alisema hayo ni ya mahafali ya kwanza kwa wanafunzi hao ambao waliokolewa katika ndoa na kurudishwa shuleni kupitia mfumo wa elimu Masafa ‘Elimu ya watu wazima’. 
“Wahitimu ni wanafunzi ambao historia yao ya elimu ilihuishwa mwaka 2014 baada ya kuokolewa katika ndoa na kurudishwa shule kupitia mfumo usio rasmi wa elimu ya watu wazima”,alieleza Myola. 
“Uwepo wa wanafunzi hawa ulisababisha shirika letu kuanzisha kituo cha elimu ya sekondari cha Agape Knowledge Open School chenye usajili namba IAE/OS/0273 ambao ulitolewa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima”,aliongeza Myola.
Myola aliwataka wazazi na walezi kuwasaidia watoto hao pindi watakaporudi nyumbani kupumzika wakati wakisubiri matokeo ya na kuwakumbusha kuwa hawarudi nyumbani kuolewa. 
“Wanaporudi nyumbani siyo kwamba wanarudi kuolewa,bado hawajamaliza masomo,watoto hawa wana uwezo mkubwa darasani,tuna imani watafaulu vyema katika mtihani wao,mnachotakiwa kufanya ni kuwalea katika ustawi unaotakiwa,msiwaache peke yao,msiwaozeshe”,alisema Myola. 
Katika risala yao kwa mgeni rasmi,wahitimu hao walisema elimu waliyoipata imewapatia msingi mzuri wa kujiunga na elimu ya juu lakini pia imewajengea uwezo mzuri wa kujitambua,kufikiri,kufanya maamuzi sahihi na mambo kadha wa kadha ikiwemo elimu ya ujasiriamali,stadi za maisha na stadi za kazi na afya ya uzazi. 
Wahitimu hao pia walipaza sauti kuhusu kesi zao kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia kwamba kesi zinachukua muda mrefu pasipo sababu za msingi na mwisho wake unakuwa haueleweki. 
“Tunaomba kesi za watoto zinazofikshwa katika vyombo vya sheria haki itendeke,kesi nyingi zinazohusu watoto zimekuwa zikichezewa sana na kuwa na mwisho mbaya hasa za mimba,kubakwa,vipigo,kutelekezwa ili ukweli ujulikane na haki ya mtoto ipatikane”,ilieleza sehemu ya risala yao. 
Wahitimu hao pia walitaka wazazi wanaolazimisha watoto waolewe na wanaume wanaotia mimba wapatiwe adhabu kali na wanapofikishwa mahakamani kesi zao zisichukue muda mrefu kama sheria zinavyoelekeza. 
Aidha waliyaomba mashirika mbalimbali kushirikiana na shirika la AGAPE linalomjali,kumlinda,kumthamini na kumsaidia mtoto wa kike katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia,ndoa na mimba za utotoni mkoani Shinyanga. 
Akizungumza katika mahafali hayo,Mgeni rasmi James Malima alisema serikali inatambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na shirika la AGAPE katika kumkomboa motto wa kike kielimu na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata elimu. 
“Watoto wa kike wanapitia changamoto nyingi,kinachotakiwa wazazi na walezi pamoja na jamii kwa ujumla tushirikiane kuwalinda watoto wa kike na tuwapatie elimu,mtoto anapaswa kwenda shule siyo kuozeshwa”,alisema Malima. 
Hata hivyo aliwataka wazazi kuacha tabia ya kuozesha watoto kwa tamaa ya mali na wengine kuwapeleka katika nyumba za watu kufanya kazi za ndani bali wawapeleke shule ili waweze kutimiza ndoto zao. 
Wahitimu 29 wa kidato cha nne shule ya Sekondari Agape Knowledge Open School wakiingia ukumbini wakati wa mahafali ya kwanza katika shule hiyo Ijumaa Oktoba 20,2017- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Maandamano kuelekea ukumbini 
Mgeni rasmi na viongozi mbalimbali wakiwa katika maandamano kuelekea ukumbini
Mgeni rasmi ,Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Shinyanga,James Malima kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Agape Knowledge Open School
Wahitimu wa kidato cha nne wakiimba wakati wa mahafali hayo
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP),John Myola akizungumza wakati wa mahafali hayo ambapo aliwataka wazazi kuacha tabia ya kuozesha watoto kwa tamaa ya mali na badala yake wawapeleke shule
Wahitimu wakifurahia jambo wakati Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP),John Myola akizungumza.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP),John Myola akisisitiza "Mtoto wa Kike Shule"
Mwenyekiti wa mtaa wa Busambilo kata ya Chibe ilipo shule ya  Agape Knowledge Open School Charles Mayunga akilishukuru shirika hilo kwa kuwapa elimu watoto ambao wameokolewa katika ndoa
Wanafunzi wanaobaki wanaosoma katika shule ya Agape Knowledge Open School wakiimba wimbo kulishukuru shirika la AGAPE jinsi linavyosaidia watoto wa kike
Mkuu wa shule  ya sekondari Agape Knowledge Open School ,Adili Haruni Nyaluke akielezea historia ya shule hiyo
Wanawake waliopatiwa elimu ya ujasiriamali na shirika la AGAPE wakiimba na kucheza wakati wa mahafali hayo
Wazazi na walezi wakiwa katika mahafali hayo
Wahitimu wa kidato cha nne wakiwa ukumbini
Wahitimu wa kidato cha nne wakiimba na kucheza
Wahitimu wakiimba wakati wa mahafali hayo
Wageni waalikwa wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea wakati wa mahafali hayo
Wazazi na wageni waalikwa wakiwa katika eneo la tukio
Wanafunzi kutoka shule ya Sekondari Tinde wakiwa katika mahafali hayo

No comments: