Advertisements

Sunday, March 11, 2018

Vigogo wanne wa dawa za kulevya wakamatwa

Vigogo wanne, wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanaodaiwa kushirikiana na wanasiasa wakubwa serikalini wamekamatwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya aina ya heroine.
Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA), Luteni Kanali Federick Milanzi alisema hayo juzi katika mahojiano maalumu na mwandishi wetu yaliyofanyika katika ofisi za tume hiyo.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wiki iliyopita. Hata hivyo, Kamishna Milanzi hakuwataja majina wala kiasi cha dawa walizokamatwa nazo kuwa bado zipo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Alisema watuhumiwa hao walikuwa na mawasiliano na baadhi ya viongozi wa juu wa serikalini na kwamba wanashikiliwa huku uchunguzi ukiendelea.
“Hatuwezi kuwaachia hadi uchunguzi ukamilike... taratibu za Mkemia Mkuu zikikamilika watafikishwa mahakamani,” alisema.
Kamishna huyo alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumefanikiwa baada ya kudhibitiwa kwa mianya waliyokuwa wanatumia kupitishia dawa hizo ikiwamo katika viwanja vya ndege, mipakani na Pwani ya Bahari ya Hindi.
Alisema wafanyabiashara hao walikuwa wanaitumia Tanzania kupitisha dawa za kulevya na kuzipeleka nchi mbalimbali ikiwamo Afrika Kusini na China.



Mbinu mpya
Kadhalika, Kamishna Milanzi alizungumzia mbinu mpya zinazotumiwa na wafanyabishara hao kusafirisha dawa hizo.
Alisema wanatumia majahazi kupitisha hasa katika eneo la Kilambo mkoani Mtwara unakopita Mto Ruvuma mpakani na Msumbiji.
“Watu wa Serikali walikuwa hawajabaini eneo hilo kama linatumika kupitishia dawa za kulevya na zilikuwa zinaingizwa kwa kiasi kikubwa hivyo sasa hivi kila mtu anayepita eneo hilo tunakagua hati yake ya kusafiria, mizigo na vyombo vyote vya usafiri,” alisema.
Pia alisema kuna wafanyabiashara wa kemikali bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya ambao hawajasajiliwa na wanaingiza dawa hizo kinyemela huku matumizi yake yakiwa siyo halali.
“Mamlaka inadhibiti uchepushwaji wa kemikali hizo ili zisitumike vibaya kutengenezea dawa za kulevya,” alisema.
Alisema wafanyabiashara hao wanatakiwa kufuata taratibu wanapotaka kuingiza kemikali hizo nchini ikiwamo kusajiliwa na kupata vibali kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Sasa hivi tumedhibiti mipaka yote ya nchini ikiwamo viwanja vya ndege. Kwa maeneo ya Pwani ya bahari tupo pale saa 24, kazi yetu ni kukagua meli na majahazi yote. Kwa mfano, sasa hivi meli za uvuvi zimepungua tofauti na mwanzo zilikuwa zinaingia nyingi. Hapa tunaona kulikuwa kuna kitu kinaendelea,” alisema Milanzi.

Sheria mpya
Lakini kupungua huko hakutokani na udhibiti huo pekee kwani Kamishna wa Sheria DCEA, Edwin Kakolaki alisema sheria mpya iliyopitishwa Desemba 2017 ambayo inasema mtu anayekutwa na gramu 20 za dawa za kulevya aina ya cocaine au heroine hapati dhamana na akipatikana na hatia anahukumiwa kifungo cha maisha na mali kutaifishwa imewaogopesha baadhi ya wahalifu hao na kuamua kuachana na biashara ya dawa za kulevya kwa kuhofia kutaifishwa mali zao na kufungwa maisha.
“Ndiyo maana unaona sasa hivi kuna uhaba wa dawa hizo na hata watumiaji sasa wengi wanakwenda kwenye vituo vya tiba ya kuondoa uraibu au methadone,” alisema.
Mpaka sasa vituo zaidi ya vitano vimefunguliwa kwa ajili kupata tiba hiyo katika hospitali za Mwananyamala, Temeke, Muhimbili, Mbeya na mkoani Mwanza na jumla ya watumiaji 5,500 wa dawa za kulevya wanapatiwa tiba.

Jinsi zinavyoteketezwa
Hivi umewahi kujiuliza dawa za kulevya zinazokamatwa hupelekwa wapi?
Hayo yanajibiwa na Kamishna Kakolaki ambaye anasema dawa hizo huteketezwa katika mitambo ya kuzalisha saruji katika viwanda mbalimbali nchini.
“Uchomaji wa dawa hizi ni mgumu kidogo utakapounguza kwenye moto wa kawaida haziungui zote nia na madhumuni ziteketee kabisa ndiyo maana tunaunguza kwenye viwanda vya saruji kwani moto wake ni nyuzi joto 500,” alisema Kakolaki.
Alisema uchomaji huo hushuhudiwa na mamlaka hiyo, mwendesha mashtaka wa Serikali, jaji, maofisa wa mazingira, polisi na Usalama wa Taifa.
Alisema kwa kawaida kielelezo kinapotolewa mahakamani na kesi ikiisha, Mahakama hutoa amri ya kukiteketeza.
Hata hivyo, alisema wakati mwingine vielelezo huteketezwa hata kabla kesi haijaisha kutokana na kuwa kikubwa.
“Kwa mfano, Januari 27 walikamata magunia ya bangi yenye uzito wa kilo 6,703 yalilazimika kuteketezwa kutokana na mazingira magumu ya kutunza kielelezo,” alisema na kuongeza:
“Magunia hayo yangeweza kuibwa, kunyeshewa mvua hivyo kwa kuangalia mazingira hayo mpelelezi ameomba mahakamani kuteketeza.”
Ili kuweka ushahidi, polisi, hakimu au jaji hushuhudia na kuweka utaratibu wa kimaandishi na wa picha kuwa kielelezo kimeteketezwa.
“Utaratibu huo hufanyika katika heroine na cocaine pia,” alisema.

Chanzo: Mwananchi

No comments: